Wednesday, February 15, 2012

IFAHAMU HISTORIA YAKO KABLA YA KUWA MTUMWA KWENU

Mambo vip wadau wa blog yetu...?? Natumaini weekend yenu ilikwenda vizuri na tuko na afya njema pamoja na wenzetu tuwapendao. Kama kuna mtu anaumwa au kuuguliwa na ampendaye basi tunawaombea ahueni ili tuendeleze gurudumu la maendeleo la maisha yetu binafsi, wanaotuzunguuka na taifa letu kwa ujumla.
Siku ya jumamosi nilipata wasaa wa kwenda kutembelea mji wa bagamoyo na kujua historia mbalimbali za mji ule... Kuna vitu vingi sana nilijifunza kupitia safari yangu hii na pia kuupata huo usemi uliokuwa hapo juu wa IFAHAMU HISTORIA YAKO KABLA YA KUWA MTUMWA KWENU.
Kitu cha kwanza baada ya kufika bagamoyo, ilikuwa mida ya swala kwahiyo nikakimbilia msikitini uliopo pichani hapo juu nikapata jama'a pale kisha nikaelekea zangu D'Z restaurant kupata chochote kitu kabla ya kuanza kuchimbua historia ya mji huo.
Hii ndio lunch nilioipata hapo D'z restaurant kisha nikaelekea moja kwa moja mpaka CROCODILE BRANCH. Hili ni eneo ambalo wanafuga mamba wa ukubwa na umri mbalimbali.. kuanzia umri wa siku moja mpaka mamba mkubwa kabisa ambae nimemshuhudia mwenye umri wa miaka 52 ambae alikamatwa kwenye mto pangani mwaka 1998 akiwa tayari ameishi miaka 38 duniani.
Nikiwa njiani kuelekea huko CROCODILE BRANCH nilipitia kwanza CARAVAN SERAI MUSEUM ambayo ipo katikati ya mji kabisa ambapo ndipo alipokuwa akikaa wakala/agent wa waarabu wa watumwa waliokuwa wakitoka maeneo tofauti nchini kabla ya kupakiwa kwenye mitumbwi kwenda Zanzibar.


Baada ya museum ndio nikaenda zangu kuona hawa wanyama wa ajabu ambao wanaishi mpaka miaka 150 duniani. Siri moja niliyopewa hapa ni kwamba kumbe mamba akishikwa kichwani vizuri na mkiani ujanja tena unakuwa mfukoni.. Hahahahaaa, nilijifunza mengi tuu na hawa jamaa hivi karibuni wataongeza wanyama wengine kama simba, twiga, nyoka na kadhalika. Itapunguza visingizio vya watu kushindwa kwenda kufanya utalii wa ndani kwa visababu kama vya umbali na gharama.


Nilipata nafasi na mie kushika mamba.. Uoga wangu wote niliuweka mfukoni.

Huyu ndio jamaa aliyekuwa anatuzunguusha na kutupa maelezo kuhusu hawa mamba... Hawa majamaa, wakubwa wanakula mpaka kilo 450 za nyama kwa wiki. Heeeeeeeh... Nikasema bora na me niwe mamba ili niweze kugonga nyama za kutosha tuuuu.
Huyo jamaa aliyevaa jersey ya barcelona ndio alikuwa mwenyeji wangu, anaitwa Jumanne.. Alinipa story nyingi sana za mtaani kwao na maisha ya ujumla ya vijana wa pale pamoja na changamoto wanazozipata kama vijana. Kwa kweli alinifungua macho kwenye mambo mengi na tukakubaliana next time nikienda tuonane ili tuongelee kwa upana zaidi maisha ya kawaida..

Baada ya CROCODILE BRANCH nikaelekea zangu hapa, kwenye magofu ya KAOLE. Hapa nilipata hasaa historia ya bagamoyo kwamba makabila asilia hapa ni WAKWERE( kabila la Mr. President), WAZARAMO na WADOE lakini kutokana na muingiliano wa kindoa na kimazingira kuna makabila kama WAZIGUA( akina sie sasa hawa) pia wapo mji huuu pamoja na makabila mengine. Neno KAOLE limetokana na lugha asilia ya wakwere " Shite shikalole" likimaanisha twende tukaone.. Wakati huo walikuwa wakija eneo hili kuja kuwashangaa WASHIRAZI walipokuwa wakiadhini kwa kupaza sauti wakati wa swala. WASHIRAZI walishindwa kusema "shite shikalole" wakaishia kusema KAOLE pekee.

Huu ndio msikiti wa WASHIRAZI amabao ulijengwa karne ya 13 na ndio uliokuwa unakuja kushangawa na makabila wenyeji wa bagamoyo. Hizo ngazi unazoziona hapo mbele ndio sehemu ambayo mtu akitaka kuadhini anapanda juu na kutoa adhana.


Hili ni kaburi la DARWESH.. Hili si jina halisi la aliyezikwa hapa, bali ni cheo alichokuwa nacho. DARWESH maana yake ni kiongozi wa mstari wa mbele kwenye mapambano ya kueneza dini ambayo ilikuwa uislamu kwa WASHIRAZI.


Hiki ndio kisima al-maarufu sana cha SHARIFA na si SHARIFU kama wengi wetu tulivyokuwa tukisikia. Kisima hiki watu huja kunywa maji yake na wengine kuoga ili kuondoa mikosi na balaa maishani mwao. Kisima hiki hakijawahi kukauka tangu kujengwa kwake karne ya 13 na ajabu zaidi ni kwamba kinatoa maji baridi(yasiyokuwa na chumvi) japokuwa kimechimbwa kandokando ya bahari. Umaarufu zaidi pia ni kutokana na historia ya SHARIFA mwenyewe ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 13 na alikuwa ni mtabiri wa mambo mbalimbali. Siku aliyofariki, walifariki pia watoto wengine watatu ikiaminika kwamba walikuwa wakimsindikiza SHARIFA.





Hili ndio kaburi la SHARIFA( lilijengwa kama nyumba) pembeni likiwa limezungukwa na makaburi ya hao watoto wengine watatu waliomsindikiza.

Hili ni kaburi la Sheikh Ali bin Jumaa amabaye alizaliwa mwaka 1215 na kufariki 1270. Huo kama mlingoti mbele ya kaburi ulikuwa ukijengwa kama ishara ya cheo ulichonacho kwenye jamii. Jinsi huo mlingoti unavyokuwa mrefu ndio inaonesha jinsi gani cheo cha mtu.


Kaburi la wapendanao hilo... Watu huja pia hapa na kuomba dua wakiamini kupata baraka kwenye ndoa zao na mahusiano yao pia.


Huu ni msingi wa nyumba iliyojengwa na washirazi karne ya 13.. Ilichimbuliwa tena na muingereza aliyeitwa Dr. Neville Chirtick mwaka 1958.


Huu ni msikiti mwingine wa washirazi.. Ulijengwa karne ya 15


Nikaenda pia MSALABANI.. Hii ilikuwa ni alama iliyowekwa na wakatoliki wakat walipokuwa wamejenga kanisa lao la kwanza la kikatoliki afrika mashariki


Na hili ndio kanisa lenyewe


Huu ni mbuyu ulipandwa kama alama ya ufunguzi wam kanisa hili la wakatoliki.. Ulipandwa mwaka 1868 na pia ni maarufu kwa kuwa umekuwa ukiongezeka upana na hadi mara ya mwisho kupimwa ulikuwa na upana zaidi ya mita 12. Pia kuna mnyororo ambao ulitumika kufungia punda karne hiyo..


Wakati nikiwa kwenye safari yangu hii ya kuchimbua historia, pia nilipata bahati ya kukumbana na DINA MARIOS mtangazaji maarufu wa clouds fm akifanya shooting ya kipindi chake cha LEO TENA. Hatukuongea kwasababu nilimkuta yupo kati kati ya shooting lakini nilipenda kupata wasaa tukabadilishana mawili matatu maana nae kama kijana nadhani angeweza kutusaidia mchango wa mawazo namna ya kuimarisha blog yetu.

Kwa picha zaidi ya safari hii yangu ya BAGAMOYO.. Tafadhali tembelea ukurasa wangu wa facebook kisha angalia photos zangu kwenye albamu ya BAGAMOYO EXPLORATION utapata zilizobaki ambazo sikupata muda wa kuziweka hapa.

Shukrani sana kwa mshkaji wangu JUMANNE... Aliniwezesha sana kupata burudani ya bagamoyo.

STAY TUNED.... KUNA TRIP YA TANGA NA ZANZIBAR, PHOTOS ZITAKUJA HAPA AS SOON AS POSSIBLE BAADA YA SAFARI HIZO.!!!!!